Viongozi wa Zambia na Tanzania wasisitiza dhamira ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili
2023-10-26 09:56:07| CRI

Marais wa Zambia na Tanzania wamesisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Hakainde Hichilema na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwepo nchini humo kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, walisema hayo wakati wa mkutano wao pamoja na wanahabari kufuatia mazungumzo baina ya nchi hizo mbili.

Viongozi hao pia walishuhudia utiaji saini wa hati nane za Makubaliano ya Maelewano yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta tofauti, zikiwemo nishati, uchukuzi, ulinzi na afya. Katika hotuba yake, rais wa Tanzania aliahidi kujitolea kwa serikali yake katika kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa mama Samia, nchi hizo mbili zilikabiliwa na changamoto za kibiashara na vifaa hapo awali akitumai kuwa makubaliano hayo yatasaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa upande wake, Hichilema alisema yuko tayari kuona utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa, ambayo itaongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisisitiza kuwa utiaji saini wa mikataba hiyo haufai kubaki kwenye karatasi, bali nchi hizo mbili zihakikishe utekelezaji wa yale yaliyofikiwa ili kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.