AU yatoa wito tena wa "kuondolewa vikwazo mara moja, bila masharti" dhidi ya Zimbabwe
2023-10-26 09:49:16| CRI

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa kuondolewa vikwazo vyote "mara moja na bila masharti" vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika siku ya Jumatano ilisema mwenyekiti Faki "kwa mara nyingine tena anasisitiza madai ya muda mrefu ya Umoja huo ya kuondolewa vikwazo mara moja na bila masharti vilivyowekwa dhidi ya taasisi na watu binafsi wa Jamhuri ya Zimbabwe.

Mwenyekiti huyo pia ameelezea kuwa Umoja wa Afrika "unaunga mkono kikamilifu" msimamo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu suala hilo.

Mwaka 2019, jumuiya ya SADC ilitangaza Oktoba 25 kama "Siku ya Kupinga Vikwazo" kwa nchi wanachama kusimama kidete na Zimbabwe na kutoa wito wa kuondolewa vikwazo bila masharti.

Faki ameeleza kusikitishwa na athari mbaya za vikwazo vinavyoendelea kwa jamii na uchumi nchini Zimbabwe huku kukiwa na matatizo ya chakula na nishati duniani, ikiwa ni pamoja na juhudi za kujifufua baada ya Covid-19.