Xi akutana na gavana wa jimbo la California, Marekani
2023-10-26 09:54:15| CRI

Rais Xi Jinping wa China Jumatano alikutana na gavana wa jimbo la California la Marekani, Gavin Newsom, katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano mjini Beijing.

Katika mazungumzo yao alisema China na Marekani, zikiwa nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, zinachangia zaidi ya theluthi moja ya uchumi wa dunia na karibu robo ya watu wote duniani, huku biashara kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni takriban moja ya tano ya jumla ya uchumi wa dunia, ambapo maslahi ya pande zote mbili yanafungamana kwa karibu.

Xi alibainisha kuwa mafanikio ya uhusiano kati ya China na Marekani hayakuja kwa urahisi na yanapaswa kuthaminiwa zaidi. Sera ya China kuhusu Marekani ni thabiti, ambayo ni kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kunufaishana, na kuongeza kuwa China itaendelea kufanya kazi katika mwelekeo huu ikitumai Marekani itashirikiana na China katika mwelekeo huo huo.

Naye Newsom amesema, katika miongo michache iliyopita, China imepata mafanikio makubwa katika maendeleo, hasa katika nyanja ya nishati mpya. Amesisitiza kuwa hakuna uhusiano mwingine wa nchi mbili ambao ni muhimu zaidi kuliko huu kati ya Marekani na China, na uhusiano huu ni muhimu kwa mustakabali wa Marekani na unahusu ustawi wa watu wake.