Mahakama ya Juu nchini Nigeria yaidhinisha ushindi wa rais kwenye uchaguzi
2023-10-27 10:10:19| CRI

Mahakama ya juu zaidi ya Nigeria Alhamisi iliidhinisha uamuzi wa tume ya uchaguzi ambayo awali ilithibitisha ushindi wa Rais Bola Tinubu katika uchaguzi wa rais uliofanyika Februari mwaka huu katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Uamuzi wa mahakama hiyo ya juu, ambao ulitolewa kwa kauli moja na jopo la majaji saba, ulikuja baada ya miezi kadhaa ya mabishano ya kisheria. Kesi hiyo ilifikishwa katika mahakama ya juu nchini Nigeria na chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP) na Labour Party (LP), ambavyo vilidai kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa uchaguzi.

Mahakama hiyo ilitupilia mbali madai ya vyama vya upinzani na kuamua kuwa Tinubu alichaguliwa kihalali kuwa rais wa Nigeria, baada ya kukidhi matakwa ya kikatiba kama yalivyowekwa na sheria.

Abubakar Atiku wa chama cha PDP na Peter Obi wa chama cha LP, ambao waliibuka wa pili na wa tatu mtawalia katika uchaguzi wa rais alioshinda Tinubu, walikwenda mahakamani kufuta matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Tinubu alitangazwa kushinda kwa zaidi ya kura milioni 8.7 huku Atiku na Obi wakipata zaidi ya kura milioni 6.9 na milioni 6.1 mtawalia.