China kuendelea kuhimiza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Tanzania
2023-10-27 10:06:10| CRI

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, ametangaza kuwa China inatarajia kuendelea kukuza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Tanzania, ili kuelekea kwa pamoja kwenye mustakabali mzuri wa kisasa.

Chen aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo alifahamisha matokeo ya Mkutano wa Tatu wa Kilele wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja uliomalizika wiki iliyopita mjini Beijing, China.

Ameelezea maendeleo yaliyopatikana katika ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye Ukanda Mmoja, Njia Moja katika muongo mmoja uliopita, hasa katika maendeleo ya miundombinu, uchumi na biashara, uwekezaji na mawasiliano kati ya watu na watu.

Chen ametoa wito kwa nchi hizo mbili kutumia nguvu ya muunganiko wa miundombinu, kuongeza mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi, na kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana katika maendeleo ya kijani, uchumi wa kidijitali na uchumi wa bluu.

Chen amesema mwaka 2024 China na Tanzania zitaadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi, akisema China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja ili kutatua changamoto na kutafuta maendeleo ya pande zote mbili.