Kenya Alhamis ilizindua bidhaa mpya za utalii zitakazowezesha nchi hiyo kuongeza ujio wa watalii wa kimataifa.
Akiongea na wanahabari mjini Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii John Ololtuaa, alisema bidhaa mpya 17 za utalii zitaoneshwa kwa dunia na kwamba nchi hiyo ina mengi zaidi ya kutoa kwa wageni wanaokwenda tena na wale wanaokwenda kwa mara ya kwanza ikiwa mbali na kwenda kuangalia wanyamapori na fukwe safi bali pia watapata kuogelea na pomboo, kupanda maputo, kutembelea mashamba ya kahawa na chai, pamoja na kujipatia uzoefu wa utamaduni na makabila ya asili ya Kenya.
Afisa huyo alibainisha kuwa mahitaji ya bidhaa mpya na nyingine yamekuwa yakiongezeka, jambo ambalo limeifanya Kenya kuelekeza nguvu zake katika kuboresha mapato yanayotokana na utalii kwa kuzingatia msimu wa wageni wa kimataifa.
Takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya zinaonesha kuwa utalii ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya mapato ya fedha za kigeni pamoja na uhamishaji wa fedha kutoka nje ya nchi, kilimo cha bustani na mauzo ya chai.