Umuhimu wa Elimu kwa Mtoto wa Kike
2023-10-28 09:00:05| CRI

October 11 ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku hiyo ni "Haki zetu ni Hatma Yetu: Wakati ni Sasa". Hivi karibuni, Mke wa Rais wa China, Peng Liyuan na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Audrey Azoulay, walihudhuria hafla ya utoaji Tuzo za UNESCO za Elimu ya Wasichana na Wanawake za 2023 hapa mjini Beijing. Peng, ambaye pia mjumbe maalum wa UNESCO kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya wasichana na wanawake, na Azoulay kwanza walitoa tuzo kwa wawakilishi walioshinda tuzo wa Mfuko wa Watoto na Vijana wa China (CCTF) na Muungano wa Pakistani wa Elimu ya Wasichana (PAGE).

Katika hotuba yake, Mama Peng alisema ushirikiano wa karibu wa China na UNESCO, hasa uanzishwaji wa tuzo ya elimu ya wasichana na wanawake umekuwa mfano, umetoa uzoefu wa thamani na kubeba jukumu la kupigiwa mfano katika maendeleo ya elimu ya wasichana na wanawake duniani kote. Alibainisha kuwa elimu ya wasichana na wanawake inakabiliwa na hali, mahitaji na changamoto mpya katika ulimwengu wa leo, na kutoa wito kwa pande zote kuongeza zaidi michango na uungaji mkono wao, kuendeleza kikamilifu elimu za afya, dijitali na sayansi kwa wanawake, na kuwasaidia wanawake zaidi kuboresha afya zao pamoja na kuimarisha uwezo wao wa kuvumbua na kuanzisha biashara. Katika kipindi cha Ukumbi wa wanawake leo hii tunajadili umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.