Kiongozi wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan amesema, jeshi la nchi hiyo halitakuwa sehemu ya mchakato wowote wa kisiasa katika siku za baadaye, wala kuingilia katika uongozi wa serikali huru ya mpito ya nchi hiyo.
Jenerali Al-Burhan amesema hayo alipompokea Mjumbe Maalum wa Uswis katika Pembe ya Afrika, Sylvain Astier katika mji mkuu wa mkoa wa Bahari Nyekundu, Port Sudan, jana jumapili.
Taarifa iliyotolewa na Baraza hilo imesema, mkutano huo ulijadili umuhimu wa kuunda serikali huru itakayosimamia kipindi cha mpito nchini humo kabla ya kufanya uchaguzi mkuu.
Pia mkutano huo ulijadili juhudi za ndani na nje kumaliza mapigano yanayoendelea nchini humo, mazingira ya kibinadamu, na njia za kuwezesha kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahitaji.