Uganda na China zasaini makubaliano ya kuendeleza matumizi ya internet nchini Uganda
2023-10-31 14:22:46| cri

Uganda na China zimesaini makubaliano ya kukuza maendeleo, ushirikiano na mageuzi ya kidijitali nchini Uganda. Makubaliano hayo yamesainiwa mjini Beijing, ambako kongamano la ushirikiano wa kujenga uwezo wa kidijitali kati ya China na Afrika linafanyika.

Waziri wa Habari, Teknolojia ya Mawasiliano na Mwongozo wa Kitaifa wa Uganda Dkt. Chris Baryomunsi, amesema serikali ya Uganda imekuwa ikishirikiana na China kuweka uti wa mgongo wa miundombinu ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya internet. Amesema China imepiga hatua kwenye teknolojia na imekuwa muhimu katika kusambaza kebo za internet nchini Uganda.

Amesema kupitia ushirikiano huu, wataweza kujenga miundombinu mipya, vifaa, mafunzo na kutoa huduma kwa waganda wote.

Dk. Baryomunsi amesema kwa sasa wanaunganisha maeneo ya mijini na vijijini kwa kutumia makampuni ya China na kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma na serikali inataka kila mtu afurahie huduma ya internet.