Israel yaendelea na mashambulio ya ardhini katika Ukanda wa Gaza
2023-10-31 08:27:01| CRI

Vikosi vya Israel jana jumatatu vimeendelea na mashambulio ya ardhini katika Ukanda wa Gaza, huku idadi ya vifo katika eneo hilo ikizidi 8,300.

Pia siku hiyo, Jeshi la Ulinzi la Israel lilitangaza kuwa, askari mmoja wa Israel aliyetekwa nyara na wapiganaji wa kundi la Hamas Oktoba 7, ameachiwa huru. Awali Jeshi hilo lilisema jumla ya watu 239 walitekwa nyara katika shambulio hilo la Hamas.

Wakati huohuo, mjumbe wa kamati ya kisiasa ya kundi la Hamas, Izzat al-Rishq, amepinga madai hayo ya Israel, na kusema yanalenga kuleta mtafaruku na kwamba hakuna anayeamini kauli za Israel.

Licha ya wito wa jamii ya kimataifa wa kumaliza mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuwaachia huru mateka, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa mapigano yataendelea.

Netanyahu amesema hayo alipozungumza na vyombo cha habari cha kigeni mjini Tel Aviv, na kusisitiza kuwa, Israel haikuanzisha vita hiyo, wala haikutaka vita, lakini itashinda vita hiyo.