Kampuni 30 za China kushiriki katika Wiki ya Mitindo ya Mavazi ya Afrika
2023-11-01 08:38:51| CRI

Kampuni 30 za China zinatarajiwa kushiriki katika Wiki ya 9 ya Maonyesho ya Ubunifu wa Mavazi ya Afrika (ASFW), ambayo itafanyika kuanzia tarehe 3 hadi 6 mwezi huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Rais wa Shirikisho la Watengenezaji wa Vitambaa na Nguo la Ethiopia, Goshu Negash amesema, maonyesho hayo ya kimataifa ya siku nne yatakutanisha zaidi ya waagizaji 300 wanaojihusisha na sekta za nguo, ngozi, teknolojia na mapambo ya ndani, na kwamba kati yao, washiriki 30 wanatoka nchini China.

Amesema maonyesho ya mwaka huu yatahusika na ajenda muhimu za sekta hiyo, ikiwemo Eneo la Biashara Huria la Afrika, uzalishaji endelevu na nafasi ya akili bandia katika maendeleo ya viwanda vya nguo na vitambaa barani Afrika.

Amesema watengenezaji wa vitambaa kutoka China wanachukua nafasi muhimu katika maendeleo ya sekta ya nguo na vitambaa ya Ethiopia, zikitoa nafasi za ajira na kuhamisha teknolojia kupitia bustani zao za viwanda zilizoko Dukem, Adama na Dire Dawa nchini Ethiopia.