Israel yaendelea na mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza
2023-11-02 08:22:20| CRI

Israel imeendelea na mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza, licha ya wito wa jamii ya kimataifa wa kusimamisha mapigano, na kusababisha kifo cha kamanda wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas katika shambulio la anga, huku kundi la kwanza la wakazi wa Gaza likiingia nchini Misri tangu kuanza kwa mapigano hayo Oktoba 7.

Jeshi la Israel limesema katika taarifa yake kuwa, ndege ya kivita ya jeshi hilo ilifanya shambulio lililosababisha kifo cha Muhammad A’sar, mkuu wa kitengo cha mizinga ambaye aliongoza mashambulio kadhaa ya makombora dhidi ya maeneo yaliyolengwa ya Israel.

Jeshi hilo pia limesema askari wake 15 wameuawa siku moja iliyopita katika matukio matatu tofauti kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Jana jumatano, kundi la kwanza la raia 500 wenye hati za kigeni za kusafiri, na watu wengine 80 waliojeruhiwa waliingia nchini Misri kupitia mpaka wa Rafah.