Wataalamu kutoka nchi 10 za Afrika wawezeshwa ujuzi wa udhibiti vifaa tiba
2023-11-02 10:03:55| cri

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya Tanzania (TMDA) imewapa mafunzo wataalam kutoka nchi 10 za Afrika kuhusu tathmini ya udhibiti wa vifaa tiba kwa ajili ya akina mama, watoto wachanga na watoto.

Wataalam hao wanatoka katika mamlaka za udhibiti wa vifaa tiba na vitendanishi za Uganda, Kenya, Ethiopia, Nigeria, Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Rwanda, Ghana, Senegal na Tanzania.

Kongamano hilo ni la kwanza Barani Afrika ambapo mafunzo hayo yanafanyika kufuatia nchi za Afrika kutokuwa na uwezo wa kudhibiti vifaa tiba kwa ajili ya akina mama na watoto, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kujenga uwezo wa kutathmini bidhaa kabla hazijaingia kwenye soko.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Mkurugenzi wa Vifaa tiba na vitendanishi Bibi Kissa Mwamwitwa amesema watabadilishana uzoefu ili kupata wataalam watakaokuwa wana uwezo wa kusaidia eneo hilo la vifaa tiba kabla havijaingia sokoni.