Reli ya TAZARA yashuhudia ongezeko la mapato
2023-11-02 08:23:00| CRI

Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imesema jana kuwa, imerekodi maboresho makubwa katika mapato ya safari za reli hiyo katika mwaka wa fedha ulioanza Julai Mosi, 2022 mpaka Juni 30 mwaka huu.

Katika taarifa yake, Mamlaka hiyo imesema maboresho makubwa ya makusanyo ya mapato yametokana na ongezeko la safari za mizigo kufuatia kufunguliwa kwa Daraja la Chambeshi mwezi Septemba, 2022. Taarifa hiyo imesema, katika mwaka huo wa fedha, mapato yaliyokusanywa yalifikia dola za kimarekani milioni 26.78, kutoka dola za kimarekani milioni 24.28 ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Wakati huohuo, idadi ya abiria waliotumia usafiri wa reli hiyo imepungua kwa asilimia moja, wakati idadi ikishuka na kufikia abiria 2,710,104 ikilinganishwa na abiria 2,738,452 iliyosajiliwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.