Gharama ya usafiri wa anga barani Afrika bado ni kikwazo kwa ukuaji wa utalii - Kagame
2023-11-03 11:13:14| cri

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema gharama kubwa za usafiri wa anga kwenda barani Afrika na ndani ya bara la Afrika, bado ni kikwazo kwa ukuaji wa sekta ya utalii, hali inayofanya kuwe na haja ya kuwepo kwa Soko la Usafiri wa Anga barani Afrika (SAATM).

Akiongea jana mjini Kigali kwenye ufunguzi rasmi wa Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (WTTC) 2023, lililowakutanisha washiriki zaidi ya 1,200, katika tasnia ya utalii duniani linaloangalia ukuaji wa sekta hiyo barani kote katika miaka ya hivi karibuni, na kuangalia changamoto zake.

Hii ni mara ya kwanza baraza hilo kufanyika barani Afrika, chini ya kaulimbiu ya 'Kujenga Madaraja kwa Mustakabali Endelevu', na kujadili ustahimilivu na ukuaji endelevu, na kuongezeka kwa athari za matumizi ya Akili bandia kwenye sekta ya utalii, na kuelewa masoko mapya na yanayoibukia.