Vikosi vya Israel vyazingira mji wa Gaza huku idadi ya vifo vya Wapalestina ikifikia 9,770
2023-11-06 08:08:27| CRI

Jeshi la Israel IDF limesema jana Jumapili vikosi vyake vilifika pwani ya mji wa Gaza na kuzingira kundi la Hamas mjini humo, wakati idadi ya vifo vya Palestina kwenye ukanda wa Gaza ikiongezeka hadi 9,770 kutokana na mashambulizi endelevu ya Israel.

Jeshi hilo limesema kupitia taarifa kuwa lengo lao ni kushambulia na kuharibu shabaha zilizochaguliwa, ikiwemo mali muhimu, vituo vya kamandi na usimamizi vya kundi la Hamas.

Msemaji wa jeshi la IDF Daniel Hagari amesema vikosi vyake vimetenganisha ukanda wa Gaza kuwa Gaza-Kaskazini na Gaza-Kusini na kudhibiti eneo la pwani, na kwamba mashambulizi makubwa yanaendelea kwenye sehemu ya kaskazini ya Gaza, ikiwemo mauaji ya makamanda wa Hamas.