Nchi za Afrika zatakiwa kutumia ushirikiano ili kuzuia hatari za kiusalama
2023-11-07 08:15:00| CRI

Umoja wa Afrika (AU) umetoa wito kwa nchi wanachama kutumia ushirikiano thabiti wa kiusalama na uratibu ili kuzuia makundi ya kigaidi na kihalifu kuweka mizizi yao katika bara la Afrika.

Akiongea mjini Nouakchott, Mauritania kwenye mkutano kuhusu usalama, ofisa mwandamizi wa Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama wa Umoja huo Alhaji Sarjoh Bah, amesema kuna haja ya kufanya juhudi za pamoja wakati matishio ya usalama yakiendelea kujitokeza na kubadilikabadilika katika sehemu mbalimbali za Afrika.

Mkutano huo uliofanyika Novemba 5-7, ulikuwa ukiangazia hali ya amani na usalama katika kanda za Sahel-Sahara na Pembe ya Afrika, ambako hali ya usalama inaendelea kuzorota, ikichangiwa na changamoto za kiutawala zinazoshuhudiwa katika baadhi ya nchi na kuzuka kwa mzozo nchini Sudan, na kusababisha ombwe la kisiasa na kiusalama pamoja na wimbi la wapiganaji wa kigeni na silaha.