China yasisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika eneo la Abyei
2023-11-07 08:51:55| CRI

Naibu mjumbe wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing amesema kudumisha amani na utulivu katika eneo la Abyei ni muhimu, China inataka Sudan imalize mapambano ya ndani haraka iwezekanavyo, na kufanya mazungumzo na Sudan Kusini, ili kuanzisha upya mchakato wa kisiasa katika eneo hilo.

Kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi Dai amesema mapambano nchini Sudan yameathiri mchakato wa kisiasa katika eneo la Abyei, na China inapongeza na kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kuhusu suala la Abyei, na kutaka jumuiya ya kimataifa kudumisha msaada ili kuepuka hali ya wasiwasi zaidi ya kibinadamu katika eneo hilo.

Abyei ni moja ya maeneo yanayogombewa na Sudan na Sudan Kusini. Mwaka 2011 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuanzisha kikosi cha usalama, ili kuhimiza nchi hizo mbili kuondoa majeshi yao katika eneo hilo.