Rais Xi Jinping wa China akutana na makamu wa Rais wa Afrika Kusini
2023-11-07 08:54:24| CRI

Rais Xi Jinping wa China amekutana na makamu wa rais wa Afrika Kusini Paul Shipokosa Mashatile katika Jumba la Mikutano ya Umma hapa Beijing.

Rais Xi amesema alipofanya ziara nchini Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka huu, alipata mapokezi ya kirafiki kutoka kwa serikali ya nchi hiyo. Mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 25 tangu China na Afrika Kusini zianzishe uhusiano wa kidiplomasia ambapo uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeingia katika “zama ya dhahabu”. Amesema China inapenda kushirikiana na Afrika Kusini kuendelea kuimarisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote na kuhimiza uhusiano huo kufikia ngazi mpya.

Makamu wa rais Mashatile, amefikisha kwa rais Xi salamu za dhati kutoka Rais Ramaphosa na kutoa shukrani kwa rais Xi kupokea nishani ya “the Order of South Africa” aliyotunukiwa, na kusema nishani hii imethibitisha mchango mkubwa wa rais Xi kwa watu wa Afrika Kusini na China, vyama viwili vya nchi hizo, na mawasiliano ya kiuchumi kati yao. Pia ameishukuru China kwa kuialika Afrika Kusini kuwa nchi mgeni wa Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) ya mwaka huu. Pia amesema Afrika Kusini inatumai kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na China.