Maambukizi ya VVU nchini Tanzania yapungua kwa asilimia 4
2023-11-08 13:53:28| cri

Kasi ya maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha UKIMWI (VVU) nchini Tanzania imepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 4.3 mwaka 2022.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchini humo, Dk Grace Magembe, kwa niaba ya Waziri wa Afya wa Tanzania, alipoongoza ujumbe wa wageni kutoka Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR). Dk Magembe ameishukuru serikali ya Marekani kwa msaada wake kupitia kwa kuendelea kushirikiana katika uboreshaji wa huduma za afya na mapambano dhidi ya VVU nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mratibu Mkuu wa masuala ya UKIMWI wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI Dk Rebecca Bunnell, ameshukuru ushirikiano unaoonyeshwa na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Pia amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, na kuahidi kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi huduma za afya.