AU yaeleza wasiwasi wake kuhusu ufadhili endelevu wa shughuli za kigaidi barani Afrika
2023-11-08 08:16:52| CRI

Tume ya Umoja wa Afrika (AU) imeeleza wasiwasi mkubwa juu ya ufadhili endelevu wa shughuli za kigaidi barani Afrika. Wasiwasi huo umeelezwa kwenye Baraza la Amani na Usalama la AU katika taarifa iliyotolewa kufuatia mkutano wake wa hivi karibuni kuhusu kukabiliana na ugaidi barani Afrika.

Taarifa imesema baraza lina wasiwasi mkubwa kuhusu ufadhili huo, hususan kuongezeka kwa uhusiano kati ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, uchimbaji haramu wa madini na maliasili, pamoja na mtiririko wa fedha haramu na athari mbaya kwa uchumi wa nchi wanachama.

Taarifa pia imesema matishio ya amani na usalama barani Afrika yanarudisha nyuma maendeleo ya kufikiwa kwa matarajio ya mpango wa maendeleo wa Ajenda 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.