Walinda amani wa UM na jeshi la DRC waanza operesheni ya pamoja dhidi ya waasi
2023-11-08 08:45:24| CRI

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema walinda amani wa Umoja wa Mataifa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameanzisha operesheni ya pamoja ya kuilinda miji miwili mashariki mwa nchi hiyo, Goma na Sake, dhidi ya wanamgambo wa kundi la M23.

Amesema hatua hiyo ni kujibu mapigano yanayoendelea kati ya wanamgambo wa M23 na makundi mengine yenye silaha katika jimbo la Kivu Kaskazini, na hatua zinazochukuliwa na kundi la M23 kuelekea mji wa Sake. Sasa maeneo salama yameshawekwa karibu na kituo cha Kitchanga ili kusaidia kuwalinda watu elfu 25 wanaotafuta hifadhi katika kituo hicho na kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu.