China yatoa msaada wa vifaa vya maabara ya kibaolojia nchini Sudan Kusini
2023-11-10 08:13:50| CRI

Kikundi cha 11 cha madaktari wa China kimekabidhi vifaa vya kisasa na vitendanishi, kusaidia maabara mpya ya kibaolojia iliyoanzishwa katika Hospitali ya Mafunzo ya Juba, nchini Sudan Kusini.

Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo Bw. Anthony Lupai, ameshukuru msaada huo na kusema maabara iliyopo katika hospitali hiyo ilikuwa inakosa vifaa hivyo kwa miaka mingi, na kusisitiza kuwa msaada uliotolewa na madaktari wa China utabadilisha upimaji na utambuzi sahihi wa magonjwa.

Meneja wa maabara hiyo Bw. Charles Mazinda amesema vifaa hivyo vitarahisisha upimaji na matibabu ya magonjwa ya kawaida kama vile malaria na homa ya matumbo ambayo kwa miaka ya nyuma ilikuwa vigumu kutambua.

Kabla ya msaada huo, upimaji wa kimaabara nchini humu ulikuwa ni mgumu na maabara chache zilizopo mjini Juba zilikuwa ghali kwa wagonjwa wanaotakiwa kupimwa mara kwa mara, kuanzishwa kwa maabara hiyo kunatoa unafuu kwa wagonjwa hao.