Okestra ya Philadelphia yaonyesha urafiki kati ya China na Marekani unaovuka bahari ya Pacific
2023-11-13 10:13:48| CRI

Novemba 10, 2023, onyesho la muziki la maadhimisho ya miaka 50 tangu safari ya kwanza ya Okestra ya Philadelphia kutembelea nchini China lilifanyika katika Kituo cha Kitaifa cha Maonyesho ya Sanaa. Katika nusu karne iliyopita, Okestra hiyo imetoa mchango mkubwa katika maelewano na uhusiano kati ya China na Marekani. Ziara hiyo ni muendelezo wa urafiki wa kimuziki ambao umedumu kwa nusu karne na watu wa China.

Mwaka 1973, Okestra ya Philadelphia ilifanya ziara ya kwanza nchini China, na kuwa balozi wa utamaduni uliovunja uhasama katika uhusiano kati ya China na Marekani katika historia. Tangu hapo, Okestra hiyo imetembelea China mara 12, na kushuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya muziki ya China, na pia kudumisha urafiki kati ya China na Marekani katika muziki.

Mpiga fidla wa Okestra hiyo, Davyd Booth anasema, uhusiano kati ya China na Marekani utakuwa mzuri Zaidi, na kwamba anaona hali hiyo inatokana na mabadilishano ya njia mbili ya kimuziki. Kwa mtazamo wake, anaona muziki ni lugha ya wote inayovuka vizuizi vya kitamaduni na kujenga madaraja kati ya watu.

Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Okestra ya Philadlphia, Matias Tarnopolsky alimwandikia barua rais wa China, Xi Jinping, kabla ya ziara yake. Anaamini kuwa ziara ya Okestra hiyo sio tu inaonyesha ishara ya mabadilishano ya kina ya kitamaduni, bali pia ni hatua muhimu katika uhusiano wa pande mbili wa kidiplomasia kati ya China na Marekani. Anasema uhusiano kati ya Okestra ya Philadelphia na China ni wa kipekee, na ni ishara ya nguvu ya muziki kutengeneza muunganiko, maelewano na uhusiano kati ya watu.

Hivi karibuni, katika majibu yake kwa barua ya Tarnopolsky, rais Xi alisisitiza kuwa muziki unavuka mipaka na utamaduni unajenga madaraja, na kueleza matumaini yake kuwa Okestra ya Philadelphia na wasanii kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo China na Marekani, watashikilia kanuni ya ustaarabu wa usawa, kufunzana, majadiliano na ujumuishi. Pia, rais Xi alitoa wito wa mawasiliano ya karibu na ushirikiano ili kukuza ustawi wa usanii, na kuendeleza ukurasa mpya wa mabadilishano ya kitamaduni na uhusiano wa kirafiki kati ya watu wa China na Marekani.

Kutokana na masuala mbalimbali kama mgogoro wa kibiashara, janga la COVID-19, vikwazo vya teknolojia ya juu dhidi ya China, na vita ya Russia na Ukraine, uhusiano wa China na Marekani umezorota kwa kasi tangu mwaka 2018. Uhusiano huo umekuwa katika ngazi ya chini Zaidi tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa pande mbili, na kuzua wasiwasi mkubwa katika jumuiya ya kimataifa kuhusu “Vita Mpya ya Baridi”.

Mwezi Novemba mwaka jana, wakuu wa nchi za China na Marekani walikutana Bali, Indonesia. Katika mkutano huo, China ilipendekeza kanuni tatu za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa Amani, na ushirikiano wa kunufaishana. Marekani pia ilitoa kauli chanya ya mambo sita yasiyotakiwa na mambo matano ya kutotiliwa maanani, ikiwemo kwamba Marekani haitafuti Vita mpya ya Baridi, haitafuti kubadili mfumo wa China, haitafuti kuimarisha wenza wa kuipinga China, haiungi mkono “ufarakanishaji wa Taiwan”, na haina nia ya kuanza mvutano na China.

Ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutoka Marekani, China haijivuni wala kujishusha, inajibu kutotendewa haki kwa uadilifu, na imejikita katika kuboresha uhusiano wa China na Marekani kuwa wa utulivu na bora Zaidi. Katika miezi ya karibuni, maofisa wa serikali ya Marekani wamefanya ziara nchini China mara nyingi, mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili yameongezeka kidhahiri, na mwelekeo wa kuwa na uhusiano mzuri unaongeza kasi hatua kwa hatua.

Kwa mujibu wa Scott Kennedy, msomi kutoka Kituo cha Elimu ya Kimataifa na Kimkakati, kuna dalili ya matumaini ya kufufuka kwa uhusiano wa pande mbili kati ya Marekani na China kutokana na mabadilishano hayo. Hata hivyo, msomi huyo anadumisha msimamo wa tahadhari kuhusu mwelekeo huo. Vilevile, Gal Luft, mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Utafiti wa Usalama wa Dunia, anakubali kuwa kuongezeka kwa mawasiliano kati ya China na Marekani kunaweza kuchangia maboresho ya uhusiano wa pande hizo mbili, na anasisitiza haja ya matokeo dhahiri kutokana na mawasiliano hayo.

Kwa bahati nzuri, katika onyesho la muziki la miaka 50 ya kumbukumbu ya ziara ya kwanza ya Okestra ya Philadelphia nchini China, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitangaza kuwa, rais wa China, Xi Jinping atakutana na rais wa Marekani Joe Biden na kuhudhuria Mkutano wa 30 wa Uchumi wa Viongozi wa nchi wanachama wa APEC utakaofanyika San Fransisco.

Hatua hii imefikiwa kutokana na maafikiano ya pande mbili ya “kurejea Bali”, lakini “njia ya kwenda San Fransisco” haitakuwa tambarare. Kama ambayo baadhi ya wataalamu wanasema, mawasiliano ya karibuni kati ya China na Marekani yanaonyesha kuwa Marekani si nguvu kuu pekee duniani, na katika kuongezeka kwa ushawishi wa China duniani, Marekani inapaswa kutafuta mtazamo mpya ili iweze kuishi pamoja na China.