Watu 38 wafariki kutokana na mafuriko nchini Kenya
2023-11-13 10:05:37| CRI

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (KRC) limesema nchi hiyo inakabiliana na athari za mafuriko yanayotokana na mvua zinazoendelea za El Nino ambazo zimesababisha vifo vya watu 38 na wengine elfu 30 kupoteza makazi yao katika wiki mbili zilizopita.

Shirika hilo limesema, mvua hizo zimewaathiri zaidi wakaazi katika maeneo kame na nusu kame kama kaunti za Tana River, Makueni, Wajir, Isiolo, Marsabit na Mandera, ambao wameathiriwa zaidi na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 40.

Katika Kaunti ya Tana River, Mto Tana ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika nyumba, mashamba, shule na nyumba za ibada, na kuwafanya mamia ya watu kuhama makazi yao, na kutafuta hifadhi kando ya barabara wakisubiri kina cha maji kupungua.

KRC imesema, idadi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko katika Kaunti ya Tana River kuwa 2,000, na Kaunti ya Garissa kuwa 20,000, huku wengi wao wakiishi katika kambi za muda.