Kituo cha kujazia gesi asilia kwenye magari chazinduliwa Dar
2023-11-13 14:16:52| cri

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania Dk. Doto Biteko, amezindua kituo cha kisasa cha kujazia gesi asilia chenye uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 800 ikiwa ni utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kuchochea matumizi nishati safi.

Uzinduzi wa kituo hicho umefanyika Novemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na mabalozi. Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk. Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uwekezaji wa sekta ya Nishati.

Dk. Biteko amesema serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) iko kwenye majadiliano na makampuni binafsi ili kujenga vituo vidogo vya Gesi ya Kusindika (LNG) ili kuweza kutoa gesi Dar es Salaam na kupeleka kwenye mikoa mbalimbali.