China yasema juhudi za pamoja zinahitajika ili uhusiano kati yake na Marekani urudi kwenye njia ya maendeleo thabiti
2023-11-14 08:54:20| CRI

China inatarajia Marekani itatimiza ahadi yake ya kutotafuta Vita vipya vya Baridi au mzozo kati yake na China, na kufanya kazi pamoja na China ili kurejesha uhusiano wa pande hizo mbili kwenye njia ya maendeleo thabiti na tulivu.

Hayo yamesemwa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning alipojibu swali kuhusu mkutano kati ya marais wa China na Marekani unaotarajiwa kufanyika wiki hii.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani ambaye hakutaja jina lake, Novemba 10 alisema malengo ya mkutano huo ni "kusimamia ushindani, kuzuia hatari ya migogoro na kuhakikisha njia za mawasiliano zinakuwa wazi".

Mao Ning amesema China tayari imetoa taarifa kuhusu ziara ya Rais Xi Jinping nchini Marekani kwa ajili ya mkutano wake na rais wa Marekani Joe Biden, na kuongeza kuwa marais hao wawili watafanya mazungumzo ya kina kuhusu masuala ya kimkakati, kiujumla na umuhimu wa kimsingi wa uhusiano kati ya China na Marekani, pamoja na masuala makuu yanayohusu amani na maendeleo ya dunia.

Mao amesema China siku zote inafuata kanuni elekezi za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani, na kufanya ushirikiano wa kunufaishana zilizopendekezwa na Rais Xi wakati wa kufuatilia na kushughulika na uhusiano na Marekani. Ushindani wa nchi kubwa hauendani na mwelekeo wa zama za hivi leo na hauwezi kutatua matatizo ya Marekani au changamoto za kimataifa.

Mao amesisitiza kuwa, China haiogopi ushindani, lakini inapinga kuelezea uhusiano kati ya China na Marekani kuwa wa ushindani, na kwamba Marekani inapaswa kuheshimu kwa dhati masuala yanayofuatiliwa na China na haki halali za kutafuta maendeleo, badala ya kusisitiza tu wasiwasi wake na kudhoofisha maslahi ya China.

Ameongeza kuwa jaribio la kuunda nchi nyingine kulingana na nia na mtindo wake ni mawazo ya kutamani tangu mwanzo, ambayo ni sifa ya kipekee ya umwamba na haitafanikiwa. China haitarajii kuibadilisha Marekani, na Marekani haipaswi kutafuta kuunda au kubadilisha China pia.

Mao amesisitiza kuwa suala la Taiwan ni suala la ndani la China, na utatuzi wa suala la Taiwan ni jambo la Wachina wenyewe na haliruhusiwi kuingiliwa na nchi za nje.