WFP yasema ukosefu wa chakula kanda ya Afrika Mashariki utaendelea hadi mwaka 2024
2023-11-14 08:48:24| CRI

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Jumatatu limesema ingawa ukosefu wa chakula huko Afrika Mashariki umepungua tangu mwaka 2022, lakini hali hiyo itaendelea kuwa mbaya hadi mwanzoni mwa mwaka 2024.

Shirika hilo limesema mapigano mapya na yanayoendelea, hali mbaya ya uchumi, na gharama kubwa ya maisha yataathiri hali ya ukosefu wa chakula na lishe katika kanda ya Afrika Mashariki. Hadi mwezi Septemba, watu takriban milioni 62.6 wako katika hali ya ukosefu wa chakula, huku Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Sudan zikiwa na hali mbaya zaidi kati ya nchi tisa za eneo hilo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatatu lilitoa ripoti mpya kuhusu hali ya ukosefu wa chakula na afya katika Pembe ya Afrika na kuonya kuwa, nchi za Pembe ya Afrika bado zinaathiriwa na hali mbaya ya hewa, ukosefu wa chakula na migogoro ya kiafya.

Kwa mujibu wa WHO, watu zaidi ya milioni 61 katika kanda hiyo wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula.