Wataalamu wa Afrika wakutana Zambia kujadili uhifadhi wa Ziwa Tanganyika
2023-11-14 08:51:18| CRI

Wataalamu kutoka nchi nne za Afrika wamekutana katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, kujadili njia endelevu za kusimamia Ziwa Tanganyika.

Wataalamu hao kutoka Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania na Zambia, wamekutana kujadili njia za kulinda na kuhifadhi anuai ya baiolojia katika Ziwa hilo na kuhakikisha matumizi endelevu ya maliasili katika Ziwa hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Kijani na Mazingira nchini Zambia, Douty Chibamba amesisitiza haja ya kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira katika Ziwa Tanganyika unaotokana na uchafuzi.

Amesema Zambia imeimarisha utekelezaji wa uvuvi endelevu na usimamizi wa misitu, ulinzi wa maeneo ya mazalio ya samaki, na kuboresha uhifadhi wa kilimo kando ya Ziwa hilo na kupata mafanikio makubwa.