Umaskini wa chakula wapungua nchini Tanzania
2023-11-15 10:31:14| cri

Naibu waziri wa fedha wa Tanzania Bwana Hamadi Chande amesema hali ya umaskini wa chakula nchini Tanzania imepungua kutokana na kuwepo kwa kiwango kizuri cha upatikanaji wa chakula.

Bwana Chande amesema hayo mjini Dar es Salaam kwenye kongamano la kujadili masuala mbalimbali yaliyojiri wakati wa utekelezaji wa tafiti zilizofadhiliwa na mradi wa benki ya Dunia kuhusu vipimo vya kiwango cha maisha ikiwa pia ni maadhimisho ya miaka 15 ya kufanya utafiti kuhusu hali ya umaskini nchini Tanzania na barani Afrika.

Amesema programu hiyo ya utafiti iliyoanza 2008 ambayo ilifadhiliwa na benki ya Dunia imeleta msaada mkubwa wa kutambua hali ya upatikanaji wa chakula nchini.

Amesema kiwango cha umasikini kwa sasa kimepungua hasa umasikini wa upatikanaji wa chakula, kwani chakula kipo kwa wingi na cha kutosha, ambapo Tanzania inaweza kuuza chakula hata kwa nchi jirani.