Watu 46 wafariki kutokana na mafuriko nchini Kenya
2023-11-15 09:24:30| CRI

Watu 46 wamefariki na maelfu ya wengine kukosa makazi kutokana na mvua kubwa ya El Nino inayonyesha nchini Kenya.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo Kithure Kindiki amesema, vifo vingi vilisababishwa na mafuriko, na kwamba jana jumanne, serikali imetoa tahadhari mpya kuhusu mafuriko.

Serikali ya Kenya imetoa tahadhari mpya katika kaunti tatu ambazo ni Garissa, Kitui, na Tana River. Mamlaka ya Maendeleo ya Mto Tana na Mto Athi (TARDA) imesema, kiwango cha maji katika mito hiyo kimepanda kwa kiasi kikubwa hadi kufikia urefu wa zaidi ya mita tano kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, na kuonya kuhusu uwezekano wa kutokea mafuriko zaidi wakati wowote.

Mkurugenzi mtendaji wa TARDA Liban Duba amesema ni muhimu kwa jamii kuzingatia maonyo yanayotolewa na mamlaka na kuhamia maeneo ya juu kwa usalama.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya imetabiri kuwa, mvua hizo zitaendelea hadi Januari, ikiashiria uharibifu zaidi ikiwa kiwango cha mvua kitaongezeka.