Rais wa China Xi Jinping ametoa wito kwa China na Marekani kutafuta njia sahihi ya kuelewana.
Hayo ameyasema wakati akiongea na mwenzake wa Marekani Joe Biden huko Filoli Estate, nyumba iliyopo takriban kilomita 40 kusini mwa San Francisco, California. Amebainisha kuwa ni ukweli usiopingika kwamba China na Marekani ni tofauti katika historia, utamaduni, mfumo wa kijamii na njia ya maendeleo. Hata hivyo amesema madhali nchi hizi zinaheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kutafuta ushirikiano wa kunufaishana, zitakuwa na uwezo kamili wa kuondokana na tofauti na kutafuta njia sahihi kwa nchi hizi mbili kuelewana, akieleza imani yake thabiti juu ya mustakabali mzuri wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Amesema uhusiano wa China na Marekani ambao ni muhimu zaidi baina ya nchi hizo mbili duniani, unapaswa kuzingatiwa na kuangaliwa katika muktadha mpana wa kasi ya mabadiliko ya kimataifa ambayo hayajaonekana katika miaka mia moja iliyopita. . Unapaswa kuendelezwa kwa njia ambayo itanufaisha watu wa nchi mbili na kutimiza wajibu wao kwa maendeleo ya binadamu.
Kwa upande wake, Biden amesema anathamini mazungumzo yake na Xi kwa sababu anaona ni muhimu kwa viongozi hao wawili kuelewana kwa uwazi, na kuongeza kuwa wanapaswa kuhakikisha kuwa ushindani usigeuke na kuwa migogoro hivyo wanapaswa kusimamia ushindani kwa uwajibikaji.
Pia amesema changamoto kubwa za kimataifa ambazo nchi hizo mbili zinakabiliana nazo, kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa, hatua za kupamabna na dawa za kulevya hadi akili bandia, zinahitaji juhudi za pamoja kutoka pande zote mbili.