China na Afrika zina mustakabali mzuri katika ushirikiano wa kilimo
2023-11-16 09:58:34| CRI

Ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika umepata matokea makubwa ukiwa na mustakabali mzuri kwa ajili ya ushirikiano wa pande zote wa kunufaishana.

Hayo yamesemwa na maofisa kwenye mkutano wa pili wa Baraza la Ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika. Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “usalama wa chakula wa Afrika: Ukurasa Mpya wa Ushirikiano wa Kilimo kati ya China na Afrika” umefanyika kuanzia jumatatu na kumalizika jana jumatano mjini Sanya, mkoani Hainan, kusini mwa China.

Waziri wa kilimo wa China Bw. Tang Renjian amehutubia mkutano huo akisema, katika muongo uliopita China imeanzisha vituo 24 vya vielelezo vya teknolojia ya kilimo barani Afrika na kueneza teknolojia zaidi ya 300 za kilimo za kisasa, na kuwanufaisha wakulima zaidi milioni 1 barani humo.

Ameongeza kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa 2021, uwekezaji wa kilimo wa makampuni ya China barani Afrika umefikia yuan bilioni 12.8 sawa na dola za kimarekani bilioni 1.77, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 11.4 kila mwaka na kuongeza zaidi ya ajira elfu 30.