Kila ploti kuwa na mita moja kulipia gharama ya umeme nchini Kenya
2023-11-16 02:16:33| cri

Wamiliki wa majumba ambayo yameunganishiwa umeme nchini Kenya sasa wana jukumu la kuhakikisha umeme unaotumiwa, umelipiwa baada ya serikali kusitisha utoaji wa mita nyingi kwa nyumba zinazomilikiwa na mtu mmoja.

Kampuni ya Kusambaza Umeme Nchini Kenya (KPLC) imechukua hatua hiyo kuhakikisha kuwa inaziba mianya ya kupoteza mapato kupitia umeme kuunganishwa kwa njia haramu.

Pia KPLC imetangaza kuwa haitaidhinisha ombi lolote la kugawa mita.

Kaimu meneja wa KPLC kuhusu ustawi wa maendeleo Kennedy Ogalo anasema Mchakato wa kugawa mita haupo na badala yake mita za sasa zitakuwa zikiunganishwa kwa mmiliki wa jumba au majumba.

Kwa mujibu wa Bw Ogalo, wamiliki wa majumba watakuwa na jukumu la kulipa gharama ya umeme ambayo imetumika kupitia mita kuu ya KPLC.

Mwongozo huo, hata hivyo, unasaza majumba ya bei nafuu yaliyojengwa na serikali na majumba yanayomilikiwa na serikali.

Ili kuhakikisha kuwa mwongozo huo mpya unatekelezwa, KPLC imekumbatia mchakato wa kudhibiti mita zote kuanzia wakati wa kutuma maombi, hadi wakati wa kutoa mita yenyewe.

Aidha, KPLC inasisitiza kuwa laini moja tu itawekwa kwa kila ombi ili kusambaza umeme kwa majumba ambayo yanamilikiwa na mtu mmoja.