Wanasayansi wa China wapanga kuongeza mavuno ya muhogo barani Afrika
2023-11-16 10:57:21| cri

Wataalamu wa kilimo wa China wamesema wanapanga kuongeza ubora wa aina mbalimbali za mihogo barani Afrika.

Wataalamu hao kutoka Akademia ya Sayansi ya Kilimo cha Kitropiki ya nchini China (CATAS) wamesema katika mpango kazi, kuwa wanapanga kutumia aina mbalimbali za mihogo na teknolojia ya juu ya kilimo katika zaidi ya ekari 500,000 za ardhi katika nchi za Afrika.

Naibu mkuu wa Chuo hicho, Xie Jianghui amesema, teknolojia hizo zinatarajiwa kuongeza mavuno ya zao hilo na kufikia zaidi ya tani 17 kwa ekari moja. Amesema taasisi hiyo itasaidia nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Nigeria, Msumbiji, na Jamhuri ya Kongo kuboresha kilimo cha aina mbalimbali za mihogo na kuongeza ngazi ya mfumo wa mashamba ya zao hilo.

Mpango huo ulitangazwa katika Mkutano wa Pili wa Ushirikiano wa China na Afrika katika Kilimo uliomalizika jana mjini San'ya, mkoa wa Hainan kusini mwa China.