China na Tanzania zazindua Karakana ya Luban ili kukuza ustadi wa vijana
2023-11-16 09:54:08| CRI

Serikali ya Tanzania imezindua karakana ya Luban ya China katika Chuo Kikuu cha Ardhi, jijini Dar es Salaam ili kukuza ustadi na shughuli za kiteknolojia kwa vijana katika taasisi hiyo ya elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa karakana ya Luban, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Adolf Mkenda amesema kuwa ujenzi wa karakana ya Luban katika Chuo Kikuu cha Ardhi ni hatua muhimu katika kukuza ujuzi wa ufundi stadi unaosaidia mipango ya maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali. Alishukuru China na Chuo cha Ufundi wa uhandisi cha Chongqing cha China kusaidia ujenzi wa karakana ya Luban, ambayo itakuza uwezo wa kuajiriwa kwa vijana waliohitimu nchini humo.

Kwa upande wake makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi Evaristo Liwa amesema karakana za Luban ni nafasi zinazoweza kuongeza usambazaji wa wafanyakazi wenye ujuzi na kupunguza utegemezi wa nje kwenye ujuzi huo, na hivyo kuongeza uwezo wa kuajiriwa kwa vijana.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Chen Mingjian amesema kuwa karakana ya Luban nchini Tanzania imejitolea kuhudumia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo, na ubalozi wa China nchini Tanzania utasaidia kikamilifu ujenzi na uendeshaji wa mradi wa karakana ya Luban nchini Tanzania, kukuza mawasiliano kati ya China na Tanzania, na kuimarisha urafiki kati ya China na Tanzania.