Xi atoa wito wa kupanua ushirikiano kati ya China na Mexico katika masuala ya fedha na magari ya umeme
2023-11-17 10:16:47| CRI

Rais Xi Jinping wa China ametoa wito wa kupanua ushirikiano kati ya China na Mexico katika masuala ya fedha, magari ya umeme na sekta nyingine zinazoibukia.

Xi alisema hayo alipokutana na mwenzake wa Mexico, Andres Manuel Lopez Obrador, kando ya Mkutano wa 30 wa Viongozi wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC). Pia alisema pande hizo mbili zinapaswa kutumia vyema utaratibu wa ushirikiano baina ya serikali na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya jadi kama vile ujenzi wa miundombinu.

Akizungumzia kuhusu urafiki kati ya China na Mexico, rais Xi amesema kwamba kwa sasa umeimarika zaidi kadiri muda unavyoenda, akibainisha kuwa mwaka jana nchi hizo mbili ziliadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia, na mwaka huu wanaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa ushirikiano wa kina na kimkakati kati ya China na Mexico.

Rais Xi alisisitiza kuwa China inaunga mkono njia ya maendeleo ya kujitegemea ya Mexico kulingana na hali yake ya kitaifa na inapenda kuimarisha mawasiliano na Mexico katika utawala wa nchi.