Mvua za El Nino zasababisha vifo vya watu zaidi ya 110 na wengine laki 7.7 kupoteza makazi katika Pembe ya Afrika
2023-11-17 10:01:39| CRI

Shirika la kimataifa la hisani la “Save the Children” limesema, mvua kubwa na mafuriko yaliyotokea katika wiki za karibuni, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 111 na wengine zaidi ya laki 7.7 wamepoteza makazi yao katika Pembe ya Afrika.

Shirika hilo lilitoa wito wa kuchukua hatua za dharura za kitaifa na za kimataifa, ili kukabiliana na tatizo kubwa la kupoteza makazi huko Kenya, Ethiopia na Somalia.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Nairobi nchini Kenya, mkurugenzi wa shirika la “Save the Children” nchini Kenya Yvonne Arunga alisema inahitajika kuongeza uungaji mkono kwa familia na watoto, ikiwa ni pamoja na kutoa habari ya kukimbilia mahali salama kabla ya mafuriko, kusaidia mipango ya kuhamisha, na kulinda miundombinu ya shule kabla ya dhoruba.