Xi asisitiza jukumu la watu kwenye uhusiano kati ya China na Marekani
2023-11-17 10:11:40| CRI

Rais wa China Xi Jinping amesisitiza jukumu la watu kwenye uhusiano kati ya China na Marekani, akisema msingi wa uhusiano, mlango wa uhusiano, hadithi za uhusiano na mustakabali wa uhusiano kati ya China na Marekani vyote vimewekwa na vitaundwa na watu wao.

Hayo amesisitiza kwenye tafrija ya kukaribishwa na mashirika ya kirafiki nchini Marekani juzi Jumatano. Amesema kuwa alikuwa anaamini kuwa mlango wa uhusiano kati ya China na Marekani ukishafunguliwa tu hauwezi kufungwa tena, na safari ya urafiki wa nchi hizo mbili ikishaanza haiwezi kukatishwa katikati.

Wakati huo huo, Xi alisisitiza kuwa Marekani haipaswi kuiona China kama mshindani wake mkuu, akibainisha kuwa China iko tayari kuwa mshirika na rafiki wa Marekani, ambapo kanuni za msingi wanazofuata katika kushughulikia uhusiano kati ya China na Marekani ni kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wa kunufaishana.

Pia rais wa China alitangaza kuwa, China iko tayari kuwaalika vijana 50,000 wa Marekani kuja nchini China kwa programu za kubadilishana na masomo katika miaka mitano ijayo ili kuongeza mawasiliano kati ya nchi hizo mbili, hasa kati ya vijana.