Bunge la Kenya laidhinisha askari polisi 1,000 kupelekwa Haiti
2023-11-17 10:24:25| CRI


 

Bunge la Kenya limeidhinisha mpango wa serikali wa kupeleka askari polisi 1,000 kusaidia kulinda usalama nchini Haiti.

Katika kura waliopiga jana asubuhi, wabunge walipitisha ripoti ya Kamati ya Pamoja ya Bunge hilo na Seneti iliyopendekeza kuwa bunge likubali ombi hilo la serikali. Polisi hao wanatarajiwa kuongoza kikosi cha walinda usalama kutoka mataifa mbalimbali (MSS) watakaopelekwa Haiti kusaidiana na vikosi vya usalama vya nchi hiyo kupambana na makundi ya wahalifu wanaovuruga usalama nchini humo.

Wabunge wametoa idhini hiyo licha ya kesi iliyowasilishwa mahakamani na kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance, Ekuru Aukot kupinga kupelekwa kwa maafisa hao Haiti, ambayo bado haijatolewa uamuzi.