Wasimamizi wa umeme wa Afrika wakutana mjini Nairobi
2023-11-17 10:04:59| CRI

Wasimamizi wa umeme wa Afrika wamekutana Nairobi, Kenya kuhimiza matumizi ya nishati endelevu katika bara hilo ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo wa siku tano umewaleta pamoja wasimamizi wa umeme kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Ghana, Namibia na Afrika Kusini, na kujadili njia ya kuharakisha matumizi ya vyanzo vya nishati safi kama njia ya kupanua utoaji wa umeme barani humo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA) Dkt James Andilile amesema nchi yake ina nia ya kupanua uzalishaji wa umeme kutoka kwenye vyanzo vya nishati endelevu. Amesisitiza kuwa, Tanzania ina bonde la ufa ambalo lina nishati kubwa ya joto la ardhini. Akibainisha kuwa faida ya nishati safi ni kwamba maendeleo ya teknolojia yamepunguza gharama za uendeleshaji wa vituo vya uzalishaji wa nishati safi.