Watu 32 wauawa katika mapigano makali ya kikabila katika mkoa wa Abyei karibu na Sudan Kusini
2023-11-20 08:54:06| CRI

Watu 32 wameuawa jana jumapili katika mapigano makali ya kikabila katika mkoa wa Abyei ulioko katika mpaka wa Sudan Kusini na Sudan.

Akizungumza na Shirika la Habari la China Xinhua, Katibu mkuu wa utawala wa Abyei, Arou Manyiel Arou amesema, mapigano hayo yalitokea mapema jana kufuatia shambulio la kulipiza kisasi kwa kabila la Ngok Dinka katika maeneo ya Wuncuei na Nyiel mkoani humo lililofanywa na vijana waliokuwa na silaha kutoka Kaunti ya Twic ya mkoa jirani wa Warrap, nchini Sudan Kusini.

Amesema shambulio la karibuni la kulipiza kisasi limetokea baada ya mapigano ya wiki iliyopita katika eneo la Ayuok kati ya pande hizo mbili, na kusababisha vifo vya watu 34, akiwemo askari wa Jeshi la Sudan Kusini. Ameongeza kuwa, pande hizo mbili zimekuwa na mvutano wa muda mrefu kugombea eneo la ardhi katika eneo la mpakani la Aneet, ambalo linatenganisha makabila hayo mawili.