Nchi za Afrika Mashariki zakubaliana kuhusu mfumo wa malipo wa kikanda
2023-11-20 22:58:45| cri

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuharakisha kuwa na mfumo wa malipo wa kuvuka mpaka ili kuongeza biashara na kupunguza gharama za ubadilishaji wa fedha mpakani.

Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano wa siku nne wa maendeleo ya miradi ya Tehama kwenye ushirikiano wa ushoroba wa kaskazini , uliofanyika wiki iliyopita mjini Nairobi.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo, timu za kiufundi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubali kuoanisha sera zao kusaidia mfumo wa malipo ya kuvuka mpaka wa kikanda.

Mfumo huo utakuwa na aina mbalimbali za malipo ya kielektroniki, ikiwa ni pamoja na uhamisho wa mtandaoni, na malipo kwa njia ya simu.

Katibu Mkuu Wizara ya ICT na Mwongozo wa Kitaifa wa Uganda Dkt Aminah Zawedde, amesema mfumo huo utaruhusu raia wa nchi wanachama kulipia bidhaa na huduma katika sarafu za nchi zao.