Nchi za Afrika zatakiwa kuongeza juhudi katika kuimarisha maendeleo ya kilimo
2023-11-21 08:45:12| CRI

Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulika na Uchumi wa Vijijini na Kilimo, Josefa Sacko amesema, nchi za Afrika zimepata maendeleo katika kuimarisha uzalishaji wa kilimo, kuboresha kilimo endelevu na kukabiliana na uhaba wa chakula na umasikini vijijini, lakini juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na suala la chakula.

Sacko amesema hayo katika mkutano wa Mawaziri wa Kilimo wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika hivi karibuni mjini Addis Ababa, Ethiopia. Ameonya kuwa, nchi zinasuasua katika kutimiza ahadi saba za Mradi wa Kina wa Maendeleo ya Kilimo barani Afrika (CAADP), ambao unalenga kuboresha maendeleo ya kilimo barani Afrika.

Amesema ukosefu wa uwekezaji, mapigano na machafuko ya ndani, na athari nyingine ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ni baadhi ya mambo yanayosababisha ukosefu wa usalama wa chakula na utapiamlo barani Afrika.