UM: Mgogoro kati ya Palestina na Israel umesababisha takriban watu milioni 1.7 kupoteza makazi yao katika Ukanda wa Gaza
2023-11-21 21:10:13| cri

Duru mpya ya mgogoro kati ya Palestina na Israel inayoendelea imesababisha idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao katika Ukanda wa Gaza. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zimeonyesha kuwa idadi ya watu waliokimbia makazi yao katika Ukanda wa Gaza imepita milioni 1.7. Chini ya kizuizi cha muda mrefu cha Israel katika Ukanda wa Gaza, hali ya kibinadamu imezorota, raslimali mbalimbali zimekosekana na hatari ya milipuko ya magonjwa ya kuambukiza imeongezeka.

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa ikisema takriban laki 9 wanaishi katika kambi 154 za makazi ya muda zilizoanzishwa na Shirika la Msaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa karibu na mashirika ya Palestina huko Ukanda wa Gaza.

Katika mgogoro huu wakazi wengi wa eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza walikimbilia kusini, lakini raslimali za ukanda wa kusini wa Gaza haziwezi kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi, na hali ya kibinadamu inatia wasiwasi. Mkurugenzi wa mambo ya dharura wa Shirika la Afya Duniani katika eneo la Mashariki ya Mediterranean Bw. Rick Brennan ametoa onyo kuhusu masuala ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, akisema kuna hatari ya kutokea milipuko ya magonjwa ya kuambukiza kama vile magonjwa ya kupumua na kuhara katika eneo la Gaza.