Mlipuko wa kipindupindu nchini Zimbabwe waamsha wito wa kufanya usafi
2023-11-21 08:43:58| CRI

Mlipuko wa kipindupindu uliotokea katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, umeamsha wito wa kuongeza hatua za kufanya usafi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo wakati mji mkuu huo ukikabiliwa na uhaba wa maji safi.

Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya kudhibiti magonjwa na magonjwa ya mlipuko mjini Harare, Michael Vere, kitovu cha mlipuko huo ni eneo lenye wakazi wengi la Kuwadzana, ambalo limeandikisha karibu nusu ya kesi za ugonjwa huo zilizoripotiwa.

Mji wa Harare umekabiliwa na changamoto ya kutoa maji safi ya bomba kwa wakazi wake, hivyo kusababisha wakazi wa mji huo kutafuta vyanzo visivyo salama vya maji. Bw. Vere amesema, maji ambayo mji huo inayapata kutoka Ziwa Chivero, ni machafu na yanahitaji kusafishwa kwa kutumia kemikali nyingi.

Waziri wa Afya na Huduma za Watoto wa nchini Zimbabwe, Douglas Mombeshora amesema, watu 12 wamefariki, saba wakitokea Kuwadzana, na kusababisha serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mlipuko huo.