Rais wa China ahudhuria kwa njia ya video Mkutano wa BRICS kuhusu suala la Palestina na Israel
2023-11-22 08:38:34| CRI

Rais wa China Xi Jinping amehudhuria kwa njia ya video Mkutano maalumu wa viongozi wa nchi za BRICS kuhusu suala la Palestina na Israel na kutoa hotuba iliyozungumzia “Kuhimiza usimamishaji wa vita na kutimiza amani na usalama wa kudumu”.

Katika hotuba yake, rais Xi amesema, mapambano yanayoendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo na majeruhi wengi. Amesema Kipaumbele kwa sasa ni kuwa pande zote zinazopambana zisimamishe vita mara moja, na kusitisha mashambulizi dhidi ya raia na kuwaachia huru raia waliokamatwa, na kuhakikisha usalama wa njia ya usafirishaji wa misaada ya kibinadamu.

Pia rais Xi amesisitiza kuwa, pande zote zinapaswa kutekeleza maazimio yanayohusika ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja huo.

Mkutano huo uliendeshwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na kushirikisha viongozi kutoka China, Brazil, Russia, Saudi Arabia, Misri, Iran, Falme za Kiarabu, Ethiopia, India na Argentina.