Ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja waimarishwa
2023-11-23 14:32:34| CRI

Ujumbe wa China kwenye Umoja wa Afrika,  Akademia ya Sayansi ya China, Shirika la Mpango Mpya wa Maendeleo ya Afrika, Shirika la Fedha la Teknolojia za Kilimo la Afrika na taasisi nyingine hivi karibuni zimetoa kwa pamoja pendekezo la “Kuimarisha Uvumbuzi wa Sayansi na Teknolojia kati ya China na Afrika, Kukuza Maendeleo Endelevu Barani Afrika” na kuimarisha zaidi ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja.

Pendekezo hilo limetolewa kwenye Kongamao la “Ushirikiano wa Kusini-Kusini: Ushirikiano na Uvumbuzi wa Sayansi na Teknolojia kati ya China na Afrika Kukuza Maendeleo ya Jamii na Uchumi Barani Afrika” ililofanyika mjini Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Wajumbe kutoka China, Umoja wa Afrika na taasisi za utafiti wa sayansi na vyuo vikuu vya Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Madagascar, Tanzania, Misri na nchi nyingine za Afrika walikusanyika ili kujadili masuala yakiwemo mabadiliko ya njia za uzalishaji wa chakula, ulinzi wa anuwai ya viumbe na usimamizi wa kisayansi wa maji.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, China na Afrika zitazindua “Mpango wa Kisayansi wa Kuhifadhi Chakula-Maji-Mazingira barani Afrika”, na kuanzisha mfumo wa mawasiliano na ushirikiano wa uvumbuzi wa kisayansi, ili kuchangia usalama wa chakula, maji na anuwai ya viumbe barani Afrika. Kufuatia pendekezo hilo, China na Afrika zitaimarisha uvumbuzi wa sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo, na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa chakula, kuvumbua mbinu za ufuatiliaji wa anuwai ya viumbe, na kuboresha usimamizi endelevu wa rasilimali ya maji barani Afrika.

Huu ni mwaka wa 10 tangu Rais Xi Jinping wa China kutoa pendekezo la kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja. Katika miaka kumi iliyopita, ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja umezidi kukubaliwa na jamii ya kimataifa, na maoni ya pamoja yameongezeka.

Kama sehemu ya jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja, jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja imekuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa uhusiano kati ya China na nchi za kikanda. Katika miaka 10 iliyopita, China na Afrika zimeanzisha njia ya kipekee ya uhusiano wa kunufaishana, na ushirikiano wao katika siasa, uchumi, utamaduni, usalama, afya na mambo mengine umepata mafanikio mazuri. Ujenzi wa pamoja wa jumuiya kati ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja umeingia katika kipindi kipya.

China na nchi za Afrika, ambazo ni nchi zinazoendelea, zitashirikiana kwa karibu zaidi ili kuhimiza maendeleo endelevu, na ujenzi wa jumuiya yao yenye hatma ya pamoja utaleta faida zaidi kwa watu wa pande zote mbili, na pia utakuwa mfano wa kuigwa kwa ujenzi wa jumuiya ya binadamu wote yenye hatma ya pamoja.