Umoja wa Mataifa wasema mpango wa kuondoka askari wake wa kulinda amani nchini DRC uko tayari
2023-11-23 08:43:55| CRI

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema, timu za pamoja za ufundi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimeandaa mpango wa kuondoa askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja huo nchini DRC (MONUSCO).

Bw. Haq amesema mpango huo wa kuondoa askari hao utafanyika kwa awamu, na utaungwa mkono na wenzi wa ndani na wa kimataifa wa DRC. Amesema kiongozi wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC Bintou Keita na naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Christophe Lutundula, wamesaini waraka wa kuondoa askari hao kwa awamu na kwa kuwajibika, ambao pia unajumuisha mpango wa muda halisi wa askari wote kuondoka nchini DRC.

Amesema mwezi Septemba mwaka huu, rais wa DRC Felix Tshisekedi alirejea tena nia ya nchi yake ya kuongeza kasi ya askari wa MONUSCO kuondoka nchini humo kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.