Mawasiliano ya mara kwa mara kati ya China na Marekani yatoa ishara chanya
2023-11-23 14:39:40| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi atafanya ziara nchini Marekani kuanzia tarehe 26 hadi 28 mwezi huu. Kabla ya hapo, tangu mwezi Juni mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani anayeshughulikia masuala ya hali ya hewa John Kerry, Waziri wa biashara wa Marekani Gina Raimondo kwa nyakati tofauti wamefanya ziara nchini China. Mawasiliano ya mara kwa mara yaliyofanywa hivi karibuni kati ya China na Marekani yameonesha ishara chanya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Jumanne wiki hii, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilieleza kuwa katika ziara yake nchini Marekani, Wang atakuwa na mazungumzo ya kina na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani kuhusu uhusiano kati ya China na Marekani na masuala ya kimataifa na ya kikanda. Pia China inataka kushirikiana na Marekani kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na marais wa nchi hizo mbili, kuongeza mawasiliano na mazungumzo, kupanua ushirikiano kwa hatua halisi, na kudhibiti maoni tofauti, ili kuhimiza uhusiano wao kurudi kwenye njia ya kawaida.

Siku hiyo hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilitangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya China Wang Yi atafanya ziara nchini Marekani. Ilisema Waziri wa Wizara hiyo Antony Blinken atazungumza na Wang kuhusu masuala mbalimbali yanayohusika na nchi hizo mbili, pamoja na mambo ya kikanda na ya kimataifa, kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kusimamia uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mbali na mawasiliano ya ngazi ya juu, hivi karibuni mawasiliano kati ya China na Marekani katika ngazi nyingine mbalimbali pia yamefanyika mara kwa mara. Jumanne wiki hii, mkutano wa kwanza wa Timu ya Uchumi ya China na Marekani ulifanyika kwa njia ya video. Pande hizo mbili zilifanya “mazungumzo ya kiujenzi ya kina na ya wazi”, kuhusu hali ya uchumi duniani, uhusiano wa kiuchumi wa nchi hizo mbili, ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za kimataifa na masuala mengine. Pia siku hiyo hiyo, Jukwaa la 10 la Xiangshan la Beijing lilifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Masuala ya China katika Ofisi ya Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani Carles amejiandikisha kuhudhuria Jukwaa hilo, ikimaanisha kwamba uhusiano kati ya majeshi ya China na Marekani ambao ulisitishwa kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya China, huenda ukaanza kuwa na mwelekeo mzuri.

Hata hivyo, Marekani haijaacha wazo lake la kupinga China. Afisa mwandamizi mmoja wa Marekani hivi majuzi alidai kuwa Marekani itajadili na China kuhusu mzozo wa Palestina na Israel na mzozo wa Russia na Ukraine, na "kuifanya China kuwa na mtazamo wa kiujenzi zaidi juu ya masuala haya mawili." Amesema kuhusu mzozo wa Palestina na Israel, Marekani "itaitaka China kushinikiza Iran kuacha kuiunga mkono Hamas." Hivi karibuni, baada ya Philippines kuanzisha mvutano na China katika Bahari ya Kusini ya China, Marekani imeeleza wazi kuunga mkono Philippines, ikidai "kuwa pamoja na Philippines".

Ziara ya Wang Yi nchini Marekani inatarajiwa kuhimiza uhusiano wa China na Marekani. Kupitia mazungumzo, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaweza kudumisha utulivu wa kimsingi. Hata hivyo, ili kurejesha uhusiano huo kuwa wa kawaida, Marekani inapaswa kuacha kabisa wazo la vita baridi, na kufanya juhudi zipaswavyo pamoja na China.